January 17, 2021

Jinsi ya kutangaza biashara yako kwa kutumia status zako za WhatsApp

Mitandao ya kijamii inazo faida tele kwenye mawasiliano kati ya marafiki na hata wanabiashara. Wengi wanaojiunga na mitandao ya kijamii huwa na malengo tofauti, ila wengi huwa na lengo la kuwasiliana na marafiki tu. Halafu kunao akina sisi, tuliojiunga kwenye mitandao ya kijamii kwa malengo la kuendeleza biashara zetu mbalimbali.

Utakubaliana nami kwamba kufikia sasa, wengi wetu tunao ufahamu wa kutangaza biashara zetu kwenye Facebook, Instagram na hata Twitter. Lakini je, unafahamu kwamba WhatsApp inao uwezo mkubwa wa kukuletea wateja katika biashara yako?

Hizi hapa mbinu saba (7) za kukuwezesha wewe kujiongezea wateja katika biashara yako:

 

1. Hakikisha unayempa namba yako amekusave

Ukipata namba ya mtu usikimbilie kuisave. Jifanye unauliza, “nikusave vipi?” Hii itamshtua na yeye akusave, hata kama alikua hana nia hiyo. Kwa kufanya hivi, utakuwa unaongeza idadi ya watu kuona statuses zako.

Kumbuka: Status zinaonekana ikiwa kila mmoja amemsave mwenzie tu! Hata kama mimi nimekusave ila wewe hujanisave, huwezi kuona status yangu.

 

2. Fungua statuses za wengine

Jitahidi kufungua statuses za wengine. Hii itawasukuma na wao kutazama za kwako.

 

3. Usipost picha nyingi.

Kama unauza viatu , si lazima upige picha kiatu kimoja kimoja. Unajaza mapicha kibao!

Fanya hivi, kusanya viatu vyako eneo moja, vipange vizuri, katika mazingira mazuri, kisha vipige picha kwa pamoja.

Picha nyingi huchosha. Na ilivyo, mtu atafungua tu labda tatu za mwanzo, kisha ataacha na kuziruka zinazofuata.

 

4. Kuwa na mpangilio

Anza picha moja, kisha fuata maelekezo (kama utahitaji kuweka). Epuka kuweka maelekezo ya bei kabla ya picha au baada ya picha.

Kwa mfano: Una picha tatu za bidhaa zako, basi weka picha moja, halafu maelekezo yako. Baadae malizia hizo picha zingine.

Wazungu husema, ‘First impression matters’. Hivyo, hakikisha picha ya mwanzo iwe ina mvuto kuliko zote! Hii itamsukuma kufungua inayofuata. Halafu vaa! Anakutana na maelekezo yako.

Bado hujamteka hapo?

 

5. Tumia caption fupi

Ukiamua kuweka maelekezo kwenye caption, basi yasiwe marefu. Caption ni yale maneno tunayopachika kwa chini ya picha.

Caption ndefu itajiweka nusu, si kila mtu ataifungua. Na ikitokea wa kuifungua, hasi hataweza kuisoma vizuri maana rangi za herufi zitafifia kwenye picha.

Hivyo tujitahidi kufupisha captions zetu za matangazo.

 

6. Jitahidi usipost matangazo kila siku

Usizoeleke kwa watu. Usiwe unapost kila kukicha matangazo tu, watu watakukariri. Jaribu kubadilikabadilika.

Unaweza ukatenga baadhi ya siku kupost vitu vingine, hasa vya kiburudani. Ukiweka kila siku statuses za matangazo tu, sie vichwa vigumu tutakukariri wewe ni wa aina hiyo. Na pengine tutaacha kuzifungua.

 

7. Tambua muda mzuri wa kupost

Muda mzuri wa kupost matangazo yako ni usiku . Hapo watu wakiamka tu, wanakutana nazo. Au upost jioni ( saa 11:30 jioni – 1:30 usiku) Imebainika kwamba asilimia kubwa ya watu hutazama statuses asubuhi tu wanapoamka au usiku kabla hawajalala.

 

Natumai kwa hayo machache, tutaufunga na kuufungua mwaka vizuri kibiashara.

Related articles