January 17, 2021

Mheshimiwa David Kadenge Dadu, MCA Malindi Town adokeza mbinu itakayotumika kumteua mbunge wa Malindi 2022

Imebakia takriban miaka miwili kufikia uchaguzi mkuu. Uchaguzi uliopita ulikumbwa na changamoto hususan katika eneo bunge la Malindi. Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa ameweka wazi azimio la kugombea kiti cha ugavana Kaunti ya Kilifi. Swali ni je, ni nani atakayemrithi?

Tulipata nafasi ya kumhoji mwakilishi wadi ya Malindi Town Mheshimiwa David Kadenge Dadu ambaye alifichua mbinu itakayotumika.

Mheshimiwa Kadenge ni nani, ulizaliwa wapi na maisha yako yalikuwa vipi wakati wa malezi yako?

Ahsante, jina langu ni mheshimiwa David Kadenge Dadu. Nilizaliwa Gede, Kaunti ya Kilifi, nikasomea shule ya msingi ya Gede kuanzia chekechea hadi darasa la nane. Nilimaliza shule ya msingi mwaka wa 1987, nikajiunga na shule ya upili ya Barani nakumaliza 1991.

Nilikuwa mtu wa kwanza kufika kidato cha nne katika jamii yetu na nilikuwa na ndugu zangu ambao nililazimika kuwasomesha. Nakumbuka vizuri tulikuwa na shamba Kanagoni ambalo tulilimia vipande (vibaruwa), tumevunja chumvi ili tupate pesa za kulipa karo, tumelima kunde tukiuza ili tulipe karo. Babangu alikuwa mgema, hivyo kufika kidato cha nne ilikuwa bahati kubwa, nililazimika kuwasaidia ndugu zangu waweze kusoma.

Baadaye nilipata kazi Casino Malindi mwaka wa 1991, na nikafanya kazi kwa mda wa miaka mitano nikafikia kiwango cha mkaguzi (inspector). Mheshimiwa Gavana Amarson Kingi alikuwa mmoja wa wale niliowasimamia. Baadaye tuliamua kugoma kufanya kazi kwa sababu ya mazingira ya kikazi, na sikurudi tena Casino. Niliajiriwa Coral Key Beach Resort mwaka wa 1994 hadi 2003 kama Front Office Manager.

Wazazi wangu hawakuweza Kunipeleka College. Hoteli ya Coral Key ilinifadhili, nikaenda kusomea Human Resource Management  Kenya Utalii College. Nimefanya kazi ya Hoteli katika maisha yangu.

Nina mke na watoto wanne, wasichana watatu na mvulana mmoja. Wasichana wawili wamehitimu shahada, mmoja bado anatarajia kuhitimu na mvulana yuko darasa la nane.

Ni nini kilikuchochea kujiunga na siasa?

Mimi ni mcha Mungu, na nashiriki kanisa la ACK ST. Andrews hapa kisumu ndogo. Na nimekuwa na ari ya kusaidia watu, nilikuwa nkisimamia nafasi ya People’s warden kanisani kuanzia 1997-2017 na nilikuwa nasimamia ustawi wa watu (people’s welfare). Nilisaidia waumini wenzangu walipokuwa  na mahitaji ya msiba, masomo, matibabu na mengineyo. Hivyo uongozi wa kanisa na waumini wenzangu, wakaona ninaweza kuwa kiongozi anayeweza kusaidia jamii. Nilitaka kuingia kwenye siasa mwaka wa 2003, lakini baada ya kuhusisha jamii yangu, hawakunibariki na kuniruhusu

Kabla ujiunge na siasa, je, kuna mradi wowote ulioufanya kwa lengo la kusaidia jamii?

Kabisaa…. Hata mbali na kanisa, hapa majengo mapya hapakuwa na maji wala stima. Mimi nilivuta bomba la maji kutoka Alaskan mpaka majengo mapya.  Mradi uliojulikana almaarufu Florida Water Project. Hata mimi nikabatizwa na kuitwa ‘Mzee Florida’. Mradi huo niliuanzisha mimi mwenyewe mpaka nikahakikisha hicho kijiji kina maji. Baadaye nilifanya mradi wa stima. Mpaka ukija kwangu utaona transformer iko karibu na nyumba yangu.

Kisha nilisomesha watoto 3 ambao niliwafadhili mpaka chuo kikuu. Mfano mzuri ni mtoto wa marehemu mama Siaya ambaye alikuwa anasoma na mwanangu darasa moja.  Mamake alipofariki, nilimchukua nikamsomesha hadi akamaliza kidato cha nne. Baadaye alijiunga na chuo cha walimu cha Shanzu na nikamlipia karo mpaka akahitimu.

Ni maswala yapi ulitaka kuyatatua au kuyabadilisha?

Swala la kwanza lilikuwa la ugawaji wa pesa za ufadhili wa masomo (Scholarship fund). Kila mwaka, kila wadi hupewa milioni kumi. Ile njia iliyokuwa inatumika kugawa ufadhili huo,  haikumsaidia mwananchi. Nimejaribu, ingawa sijafanikiwa asilimia, lakili nafikiri niko angalau asilimia themanini. Mimi hupata ripoti kutoka kwa wananchi, jinsi wanavyoona. Nina  kamati katika kila kituo cha kupiga kura huhakikisha wanatambua ni nani anastahili kupata msaada wa karo.

Huu ni mwaka wa tatu tangu uchukue wadhifa wa uwakilishi wadi, ni miradi gani ambayo umeifanya?

Nilipoingia uongozini, niliamua kumaliza miradi ambayo ilikuwa imeanzishwa na aliyekuwa mamlakani, kwa sababu hiyo ni pesa ya wananchi – ingawa hakukuwa na ubadilifu mwema wa mamlaka (proper handing over) kwa sababu za kisiasa

Mradi wa kwanza ilikuwa ni barabara ya cabro kutoka Winners Chapel kuenda Kisumu Ndogo mpaka Serena, Ngala hadi Msikitini. Mradi huo ulikuwa umeanza, na wakati wa kampeni ukasimama. Nakumbuka tulifanya maandamano, ikabidi niende kwa Gavana, akatafuta pesa na huo mradi ukaisha.

Mbona ilibidi muandamane kuishinikiza serikali ya Kaunti ishughulikie mradi huo?

Pesa ambazo zilikuwa zimepangiwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo zilitumika kwa mradi mwingine. Mwanakandarasi akashindwa kufanya kazi. Hivyo nikaamua kufuatilia kwa karibu sana na Gavana na ukakamilika.

Pia kulikuwa na mradi wa zahanati ya Kaoyeni, huo ulimalizika. Ukumbi wa Kijamii wa Mtangani (Social Hall) ambao tuliuzindua na tukaukabidhi kwa jamiii. Pia kulikuwa na shuke za chekechea za  HGM na St. Andrews, shule hizo karibuni zitakuwa tayari. Shule zengine ni za Majivuni na Kasimbiji ambazo zilikuwa hazijafunguliwa. Tulizifungua na watoto wanaendelea kusoma.

Kura ya mchujo kuwania tiketi ya ODM ilikuwaje?

Kura ya mchujo ilikumbwa na changamoto kwa sababu Kaunti ndogo ya Malindi ni ngome ya chama cha ODM. Mgombea apatapo tiketi, ni kama amefaulu nusu kuingia uongozini. Nakumbuka uchaguzi huo ulirudiwa mara tatu. Mara ya kwanza alitangazwa aliyekuwa mamlakani kuwa mshindi. Tukaenda kupinga matokeo kwa mahakama ya chama (tribunal), wakaamua uchaguzi urudiwe. Uliporudiwa, chama cha ODM kiliamua kunipea tiketi ya moja kwa moja, mwenzangu akaenda kortini na ikaamuliwa kuwa uchaguzi urudiwe. Uchaguzi ukarudiwa, nikashinda.

Kuna miswada gani ambayo umeweza kuifadhili katika bunge la Kaunti ya Kilifi?

Mswada wa kwanza ni wa mkataba wa utendaji kazi (performance contract) wa maafisa wakuu, na maafisa watendaji (chief officers and the executive).  Mfanyikazi wa Kaunti anathaminiwa kulingana na kazi anayoifanya. Niliweza kupeleka huo mswada ambao ulipita, kilichobaki ni Maafisa watendaji na kamati inayohusika na maswala ya utekelezaji waweze kuifanyia kazi sheria hiyo.

Kama Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Kazi na Huduma za Kijamii, nimekuwa na miswada ya ripoti za utendakazi katikati na mwisho wa mwaka, ambazo ni lazima kama mwenyekiti niweze kuishughulikia.

Kwa sasa tuko katika msimu mgumu wa janga la Corona, na wananchi wanapitia changamoto za kimaisha. Ni mikakati gani ambayo umeiweka kama kiongozi, kuwasaidia wananchi?

Mwanzo nawaomba wananchi waweze kufuata kanuni ambazo zimewekwa na serikali, ili kupambana na janga hili. Tumekuwa tukiskia kwa mbali lakini kwa sasa (Corona) iko Kilifi.

Niliweza kuwanunulia wananchi barakoa, lakini nilishangaa baada ya kuwagawia, walisita kuzitumia.  Ni wakati kila mmoja ajukumike. Niliwanunulia watu unga bandari 30, na nikagawia watu kupitia afisi yangu.

Kuna tuhuma kwamba wawakilishi wadi katika Kaunti ya Kilifi ‘wamewekwa mfukoni na Gavana’ kiasi kwamba wao hupitisha mapendekezo ya Gavana, wewe unasemaje kuhusu hili?

Eeeh…it’s not Eeeeh…Mimi sijui….lakini si ukweli kwa sababu bunge la Kaunti ni huru. Kazi ya Gavana ni kutekeleza yale ambayo tumeyapitisha. Tukiona ya kwamba kuna kutokuelewana sisi huwaita watekelezaji (executive) na tunawasiliana, na tukikubaliana, hatuoni haja ya kusukumana. Wao pia hutumiaa mbinu hiyo ya kujadiliana ili kusuluhisha maswala ya utendaji kazi.

Kilifi kaunti ni moja kati ya Kaunti ambazo zinaongoza kwa idadi kubwa ya mimba za mapema, na hasa wakati huu ambao wanafunzi wataendelea kubaki nyumbani mpaka mwakani. Je, ni mikakati gani ambayo umeweka ili kuhakikisha kuwa idadi hii haiongezeki hasa katika mji wa Malindi?

Mikakati yetu ni kuwaelimisha na kuwahusisha na mambo kama michezo, kuwafungulia miradi… Lakini swala hili la mimba za mapema naona si swala la viongozi pekee. Kwa sababu zamani tulikuwa tunasema ni  mikutano ya usiku (Disco) ndiyo iliyochangia mimba za mapema. Sasa hizi mimba za mapema zinatoka wapi?  Wazazi wajukumike.

Kuna uwezekano kwamba, baadhi ya matarajio ambayo wananchi wanayo kutoka kwako si majukumu yako?

Hata wale wandani wangu wa kampeni , walikuwa na matarajio mengi ambayo si majukumu ya muwakilishi wa wadi. Mimi mwenyewe nilipoingia uongozini nilikuwa na matarajio mengi.  Lakini sasa nimeona haikuwa halisi.  Kwa sababu, kupata na kutumia pesa za Kaunti ni lazima upitie  mchakato (process) mwanzo. Pale bungeni ni (kuna) fujo, na kila mmoja huvutia kwake.  Its not easy. (Si rahisi).

Wakati wa uchaguzi tuliwaahidi (watu) kazi, lakini sivyo. Kama mimi mwenyewe, ni mwenyekiti  wa kamati ya usimamizi wa kazi na huduma za kijamii, lakini nilipoingia (uongozini) nilipewa baruwa kutoka kwa kiongozi wa bajeti (Controller of budget) isemayo kwamba Kaunti ya Kilifi inapitiliza kiwango cha mishahara, nikaagizwa nitafute njia ya kupunguza matumizi hayo. Ningefanya nini?

Wananchi hupenda kumuona kiongozi wao. Mimi naishi hapa Malindi, na hata kama naenda bungeni, lazima nifike afisini nihudumie watu.  Changamoto ni kwamba mara nyengine hukosa nafasi ya kuwatembelea. Nina siku tatu za kuhudhuria vikao vya bunge, zile nyengine, mara nyengine hutumwa nje ya mji.  Watu wakiniona wanatarajia niwape pesa. Na mimi pia mara nyingine huwa sina Sasa mtu akikuona ukimuambia huna pesa, anakulaumu.  Wengine hata wanaweza wakatumia lugha ya matusi. Asilimia tisini ya matatizo ya wananchi ni matatizo ya kifedha.

Uliweza kupata wafanyikazi bandia?  Ama uliwezaje kusuluhisha tatizo hilo kama mwenyekiti?

Kweli kabisa, aah.. huo mchakato bado haujakamilika, kwa sababu tunashirikiana kama kamati ya bunge la Kaunti na halmashauri ya huduma za kwa jamii (Public Service Board). Hii ndiyo halmashauri yenye jukumu la kuajiri na kusimamisha watu kazi. Na mchakato bado unaendelea, kwa sababu tunaongozwa na sheria.

Unafikiri watu wana maoni gani kuhusu utendakazi wako? Je, unafikiri watu wanaridhika jinsi unavyowahudumia.

Mbali na kuwa na changamoto ya (petition) ombi la kupinga uchaguzi wangu, ambalo lilichukua mwaka mmoja unusu, nilikuwa nimeahidi  kujenga chuo cha mafunzo (Vocational Training Centre) hapa Malindi. Hiyo niliifuatilia kwa haraka, na karibuni tutaizindua. Pia tumejenga Kituo cha mafunzo ya teknolojia na mawasiliano (ICT Centre) Kaoyeni na maktaba ya kisasa.

Chuo cha Teknolojia na Mawasiliano cha Kaoyeni
Chuo cha ufundi cha Kaoyeni

Tunajenga Maktaba ya kisasa shule ya msingi ya central. Kulingana na mwanakandarasi, jengo hilo litakamilika mwezi wa Agosti. Tunarekebisha barabara zetu za fida. Kuna barabara ya kutoka milimani kuelekea Kasimbiji, tuliiweka kokoto. Kuna barabara ya Thalathameli kuelekea Luganje, hiyo nayo tumeitengeneza. Pia tuko na barabara ya Kosovo kuelekea Kiraho, hiyo pia tumeirekebisha. Vilevile tuko na barabara ya Alaskan kuelekea Central, hiyo pia tumeitengeneza.

Maktaba ya kisasa
Mradi wa maji na Zahanati-Kaoyeni

Mradi mkubwa ambao tuliupata ni barabara ya kwa Bobi Tuva ya Cabro, ambayo tulipata ufadhili kutoka kwa Benki ya Dunia, nashkuru niliweza kuutekeleza. Halafu tuko na barabara ya kutoka BP kupitia Alaskan, karibuni itakuwa imekamilika. Tuko na swala la tatizo la maji. Nilifanikiwa kujenga visima vinane ambavyo viko maeneo ya mashambani, nje ya mji.

Kisumu Ndogo Cabro Road

 

Alaskan – BP junction cabro road (under construction)

 

Bobi Tuva Cabro road.

 

Je, katika vituo hivi vya mafunzo, wanafunzi watalipa karo, ama Watadhaminiwa na Kaunti ya Kilifi? Ikizingatiwa kuwa huenda wengi wao walishindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya matatizo ya karo.

Kwangu nitajaribu niwezavyo ili hata kama watatakikana kulipa karo, hazina ya maendeleo ya wadi ya Malindi Town itawasimamia, hasa mwaka wa kwanza ningependa watu wasome bila malipo ili kuwapa motisha waweze kusoma

Mwaka wa 2022 utatetea kiti chako cha uwakilishi wa wadi ya Malindi Town?

Tutakuwa na mkutano hivi karibuni kati ya wawakilishi wadi wa eneo bunge la Malindi ili kumchagua atakayegombania ubunge. Wakinichagua mimi basi nitawania ubunge. Tukimpata mwingine, nitatetea kiti changu. Mbunge wa Malindi atagombea kiti cha Ugavana wa Kilifi County.

Je, unaunga mkono mchakato wa BBI?

Mimi nitaunga mkono BBI kama itazungumzia hati za umiliki wa ardhi, uchumi Baharini, Pombe ya mnazi iwe na kiwanda cha kuajiri wananchi na watu wa pwani waajiriwe kilindini.

Ni njia gani unazozitumia kuwasiliana na jamii ya Malindi Town ward?

Zamani nilikuwa nikiita mikutano ya baraza. Lakini kwa sababu ya janga la Corona, nawasiliana na watu kupitia mitandao ya kijamii. Pia mimi mwenyewe napatikana afisini mwangu.

Ungetaka kuwaambia nini wananchi wa wadi ya Malindi Town?

Nataka vijana wayajue majukumu ya muwakilishi wadi katika bunge la Kaunti. Haiwezekani mtu mmoja kutatua matatizo ya watu wote. Si njaa, mazishi, harusi, karo na mengineyo. Kila mmoja ana jukumu lake. Vijana wajihusishe na shughuli za uzalishaji wa mapato. Tuko na Mbegu Fund, watumie fursa hiyo kujinufaisha na kujiendeleza. Hakuna mtu anayeweza kumaliza matatizo ya vijana bila wao wenyewe kujishughulusha.

Related articles